Jumatatu 10 Novemba 2025 - 21:18
Gazeti la Israel lakiri uwezo wa makombora ya Iran

Hawzah/ Tathmini za upande wa Israel zinaongezeka huku zikionesha kwamba mzozo mpya kati ya Israel na Iran ni suala la muda tu, hasa ikizingatiwa kwamba Tehran imefanikiwa kuhifadhi sehemu kubwa ya mpango wake wa nyuklia.

Kwa Mujibu wa idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Tathmini za upande wa Israel zinaongezeka huku zikionesha kwamba mzozo mpya kati ya Israel na Iran ni suala la muda tu, hasa ikizingatiwa kwamba Tehran imefanikiwa kuhifadhi sehemu kubwa ya mpango wake wa nyuklia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa, licha ya mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani, hazina ya nyuklia ya Iran bado iko salama, na Tehran inaendelea kwa kasi kubwa kuboresha na kujenga upya ghala lake la makombora.

Kwa mujibu wa gazeti la Marekani New York Times, uharibifu uliosababishwa na mashambulizi yaliyoongozwa na Rais wa Marekani wa wakati huo, Donald Trump, dhidi ya Iran haukufikia kiwango cha uharibifu kamili kama ilivyodaiwa awali.

Gazeti hilo, likinukuu vyanzo vya Israel, linaripoti kwamba hifadhi ya uranium ya Iran imehamishwa katika eneo la siri, huku viwanda vya kutengeneza makombora vikiendelea kufanya kazi saa ishirini na nne kwa siku bila kukoma.

Baada ya muda wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kumalizika mwezi uliopita, vikwazo vyote vilirudishwa, na njia zote za kidiplomasia mpya zikafungwa. Tathmini zinaonesha kuwa; Iran bado inaendelea na shughuli za uboreshaji wa urani katika kituo kipya kinachoitwa “Mlima Tabar”, ambapo haijaruhusu wakaguzi wa kimataifa kuingia.

Ali Vaiz, mkurugenzi wa mradi wa Iran katika Kikundi cha Kimataifa cha Mgogoro, alisema kuwa:
“Viwanda vya Iran vinafanya kazi bila kusimama, na majibu yajayo ya Iran yatakuwa na sura tofauti; inasemekana Tehran inapanga, katika shambulio lake linalofuata, kurusha takribani makombora elfu mbili kwa wakati mmoja, badala ya makombora 500 ndani ya siku kumi na mbili, kama ilivyokuwa mwezi Juni uliopita.”

Ripoti nyingine iliyochapishwa na televisheni ya CNN inadai kwamba Iran imeanza tena uzalishaji wa makombora ya masafa marefu (ballistic missiles). Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangia mwishoni mwa mwezi Septemba, Iran imepokea kati ya shehena 10 hadi 12 kutoka China, zilizokuwa na perchlorate ya sodiamu, ambayo ni kiungo muhimu katika utengenezaji wa mafuta imara ya makombora.

Kiasi cha jumla cha malighafi hiyo kinakadiriwa kuwa takribani tani 2,000, kiwango kinachotosha kutengeneza mamia ya makombora.

Licha ya malalamiko ya Israel, China inaendelea kutuma shehena hizo, ikidai kwamba vifaa hivyo havijajumuishwa katika orodha ya bidhaa zilizopigwa marufuku na vikwazo vya kimataifa.

Taarifa za kijasusi zinaonesha kwamba Iran imerejesha hadi nusu ya ghala lake la awali la makombora (takribani makombora 2,700), na inaendelea kulipanua zaidi kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko mpya wa mapigano.

Katika mahojiano na gazeti la Financial Times, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), alithibitisha kwamba sehemu kubwa ya urani iliyoboreshwa ya Iran haikupata madhara kutokana na vita. Alidai kwamba Tehran kwa sasa inamiliki takribani kilo 400 za urani yenye kiwango cha usafi cha asilimia 60.

Pamoja na kuendelea kwa hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran, vyanzo vya Israel vinadai kwamba eneo lote liko ukingoni mwa mzozo mpya — mzozo ambao unaweza kuanza kutokana na kituo cha siri cha nyuklia au shambulio la ghafla la kombora.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha